Rais Ruto azindua na kukagua miradi ya maendeleo Kiambu

Katika ziara hiyo, Rais Ruto alizindua ujenzi wa barabara ya Kigwaru-Yamogo-Njoro yenye urefu wa kilomita nane.

Tom Mathinji
1 Min Read
Rais Ruto azindua na kukagua miradi ya maendeleo Kiambu.

Rais William Ruto amekariri kujitolea kwa serikali kufanikisha miradi ya maendeleo kwa usawa kote nchini.

Akiwahutubia wakazi wa Kiambu, baada ya kuzindua na kukagua miradi ya maendeleo, kiongozi wa taifa alisema inawezekana kutekeleza maendelo katika sehemu zote za nchi bila ubaguzi, huku akipigia debe kauli mbiu ‘Usawa ni Sawa’.

Katika ziara hiyo, Rais Ruto alizindua ujenzi wa barabara ya Kigwaru-Yamogo-Njoro yenye urefu wa kilomita nane, na barabara unganishi za Gatuikira, katika eneo bunge la Kiambaa.

“Mradi huo wa shilingi milioni 560, ni sehemu ya uwekezaji wa shilingi bilioni 60 za ujenzi wa barabara za kilomita 411 katika kaunti ya Kiambu,” alisema Rais Ruto.

Kiongozi wa taifa alisema ujenzi wa barabaa ya Mau Mau umekamilika kati ya asilimia 80 na 90, akidokeza kuwa sehemu iliyosalia inatarajiwa kukamilika mwezi Aprili mwaka 2027.

“Tutaanza ujenzi wa barabara ya Muthaiga- Kiambu kuwa yenye safu mbili mapema mwaka ujao, ili kupunguza msongamano,” aliongeza Rais Ruto.

Kwenye ziara hiyo, Rais alikuwa ameandamana na Naibu Rais Prof. Kithure Kindiki na mbunge wa Kikuyu Kimani Ichung’wa miongoni mwa viongozi wengine.

Share This Article