Wasanii Tanzania watakiwa kuzingatia usalama wa watoto

BASATA inasisitiza kuwa wasanii wana wajibu wa kulinda haki, usalama na ustawi wa watoto kwa kuepuka maudhui yanayoweza kuwaathiri kimaadili na kisaikolojia.

Marion Bosire
1 Min Read

Wasanii na waandaaji wa maudhui ya mitandaoni nchini Tanzania, wamekuwa wakipokea mafunzo kuhusu kulinda usalama wa watoto mitandaoni.

Mafunzo hayo yalifanikishwa na Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wanawake na Makundi Maalumu, Wizara ya Sanaa ya Tanzania pamoja na Baraza la Sanaa la Taifa, BASATA.

BASATA ilikumbusha wasanii na wadau wa sanaa nchini humo kuzingatia maadili na umri wa watoto wanapotengeneza kazi za sanaa na maudhui ya mitandaoni, ili kuhakikisha yanakuwa salama na yanayojenga jamii.

Afisa mwandamizi anayesimamia masuala ya sanaa katika BASATA, Abel Ndaga ndiye alitoa changamoto hiyo wakati wa mafunzo hayo ya siku mbili jijini Dar es Salaam.

BASATA inasisitiza kuwa wasanii wana wajibu wa kulinda haki, usalama na ustawi wa watoto kupitia kazi zao, kwa kuepuka maudhui yanayoweza kuwaathiri kimaadili na kisaikolojia.

Waliarifiwa kwamba ushirikiano kati ya wasanii, wazazi na jamii ni muhimu katika kuhakikisha watoto wanapata maudhui yanayofaa na yanayozingatia maadili ya Kitanzania.

Share This Article