DPP afanikisha hukumu ya kifungo cha maisha kwa mbakaji

Mshtakiwa alimdhalilisha kingono mtoto wa miaka mitatu makusudi na kinyume cha sheria, huko Kadibo, Kaunti ya Kisumu, Julai 7, 2025.

Marion Bosire
2 Min Read

Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma, DPP, amefanikiwa kuhakikisha kwamba jamaa kutoka Nyando anahukumiwa kifungo cha maisha jela baada ya kupatikana na hatia ya kumbaka mtoto wa miaka mitatu.

Hakimu Everlyne Onzere wa Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Nyando alimpata mshtakiwa na hatia ya kosa la kumdhalilisha kingono mtoto, kinyume na Kifungu cha 8(1) kikisomwa pamoja na Kifungu cha 8(2) cha Sheria ya Makosa ya Kingono ya mwaka 2006.

Upande wa mashtaka, ukiongozwa na mawakili Rodgers Morara na Douglas Moseti, pia ulikuwa umemfungulia shtaka la kufanya kitendo kisichofaa kingono na mtoto chini ya Kifungu cha 11(1) cha sheria hiyo kama shtaka mbadala.

Mahakama ilielezwa kwamba Julai 7, 2025, katika kaunti ndogo ya Kadibo, Kaunti ya Kisumu, mshtakiwa alimdhalilisha kingono mtoto huyo makusudi na kinyume cha sheria.

Mshtakiwa, aliyekuwa akifanya kazi ya kuchunga mifugo katika eneo aliloishi mtoto huyo, alimshawishi aingie nyumbani kwake kwa kisingizio cha kumpa kikombe cha chai.

Akiwa ndani, alimpa chai, akamtaka avue nguo kabla ya kumdhalilisha kingono.

Mtoto aliporudi nyumbani akivuja damu, alimweleza mamake kuhusu tukio hilo, mama akampeleka hospitalini na baadaye kuripoti kwa polisi.

Upande wa mashtaka uliwasilisha mashahidi wanne, akiwemo mtoto huyo aliyethibitisha mara tatu mbele ya mahakama kuwa alifanyiwa ukatili huo.

Baada ya kutathmini ushahidi, Hakimu Onzere alihitimisha kuwa upande wa mashtaka ulithibitisha shtaka kuu na kumtia mshtakiwa hatiani chini ya Kifungu cha 215 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai.

Mshtakiwa hata hivyo ana siki 14 kukata rufaa.

Share This Article