Raia wa Somalia amekamatwa kwa kumiliki stakabadhi za Kenya kwa njia haramu.
Khalid Hassan Ahmed, alikiri mashtaka dhidi yake na akatozwa faini ya shilingi 250,000.
Ahmed alikamatwa alipowasili katika Uwanja wa Ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta tarehe 14, Novemba, akisafiria pasipoti ya Kenya.
Kulingana na Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Ahmed pia alipatikana na pasipoti ya Somalia na kitambulisho cha taifa cha Kenya.
DCI ilisema uchunguzi ulibainisha kuwa mshtakiwa huyo alikaa nchini Kenya kinyume cha sheria, aliwasilisha kitambulisho bandia kwa maafisa wa Kenya na alitoa habari za uwongo kupata pasipoti ya Kenya.
Ahmed, ambaye alifikishwa kwenye mahakama ya JKIA, aliagizwa kurejeshwa nchini Somalia.
Wakati huo huo, mahakama iliagiza kuwa pasipoti yake ya Kenya na kitambulisho cha taifa ziwasilishwe kwa mamlaka nchini Kenya ili ziharibiwe baada ya siku 14.