Mwanamitandao wa Tanzania Mwijaku amemtetea mwanamuziki Diamond Platnumz, akieleza namna msanii huyo amekuwa na mchango mkubwa katika maisha yake licha ya kuwepo kwa kutokuelewana kati yao.
Kupitia ujumbe aliouchapisha kwenye mitandao ya kijamii, Mwijaku alimuelezea Diamond, ambaye mara nyingi humuita “Mwambino” au “Simba”, kama mtu mwenye moyo wa huruma, unyenyekevu na malezi mazuri.
Mwijaku alifichua kuwa sehemu kubwa ya mafanikio yake ya kifedha na fursa alizopata, ikiwemo safari ya Qatar na mikataba mbalimbali, zimepitia mikononi mwa Diamond.
Alikiri kuwa kutoelewana ni jambo la kawaida katika mahusiano ya kibinadamu, akisisitiza kuwa hali hiyo haifuti mchango wa Diamond katika maisha yake.
Aidha, Mwijaku alidai kuwa Diamond ana uwezo mkubwa wa kubadilisha maisha yake, huku akionyesha imani kuwa msanii huyo hatatumia ushawishi wake kumuumiza.
Akizungumzia Novemba 20, Mwijaku alisema hana maneno mengi zaidi ya kumtakia Diamond subira na kumuombea Mungu amwongoze.
Alimalizia ujumbe wake kwa kuwataka watu kuendelea kumuombea Diamond maisha marefu, akisisitiza umuhimu wa uwepo wake katika maisha ya watu wanaonufaika na mafanikio yake.
Chapisho la Mwijaku linaaminika kuwa njia ya kumshawishi Diamond amsamehe kuhusiana na ile barua ambayo mawakili wa Diamond walimwandikia wakidai fidia baada yake kudaiwa kumchafulia jina kwenye kipindi chake cha “18 za Dc”.