Serikali ya Uganda imewaamuru wafanyabiashara wanaoendesha biashara katika maduka yaliyopo chini ya ardhi “yaani basement” jijini Kampala kuondoka mara moja.
Hatua hiyo ni sehemu ya hatua za kuzuia mafuriko kama yaliyokumba jiji hilo Oktoba 2025.
Agizo hilo lilitangazwa na Waziri wa Habari, Teknolojia ya Mawasiliano na Mwongozo wa Kitaifa, Justine Kasule Lumumba, kufuatia kikao cha Baraza la Mawaziri kilichofanyika Jumatatu, Novemba 9, 2026.
Baraza la Mawaziri pia limeidhinisha shilingi za Uganda bilioni 18.99 kama fidia ya hiari kwa wafanyabiashara 1,841 waliothibitishwa kupoteza mali zao katika mafuriko ya Oktoba 30 na 31, 2025.
Aidha, shilingi bilioni 1.5 zimeidhinishwa kusaidia Shirikisho la Vyama vya Wafanyabiashara Uganda, FUTA, zikiwemo fedha za uendeshaji na mchango katika hazina yake ya mikopo ya mzunguko.
Lumumba alisema uchunguzi ulibaini kuwa mafuriko hayo yalisababishwa na mifumo ya mifereji ya maji kuzibwa na taka, ujenzi wa njia zisizo halali na shughuli za ujenzi zilizozuia maji ya mvua kuelekea kwenye mifereji mikuu.
Uchunguzi ulibaini pia kuwa baadhi ya wamiliki wa majengo waligeuza maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya maegesho ya magari kwenye basement na kuyafanya maduka, hali iliyowaweka wafanyabiashara na bidhaa zao katika hatari ya mafuriko.
Baraza la Mawaziri limeagiza Ofisi ya Waziri Mkuu, Mamlaka ya Jiji la Kampala (KCCA) na Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kuandaa mpango wa kurejesha maeneo hayo katika matumizi yake ya awali.
Taasisi hizo zimepewa mwezi mmoja kuwasilisha mpango huo, huku mamlaka husika zikielekezwa kuharakisha malipo ya fidia kwa wafanyabiashara walioathirika.