Mwanamuziki wa kike nchini Uganda Gloria Bugie amesema kwamba kamwe umaarufu hautambadilisha.
Licha ya kuwa gumzo kwenye vyombo vya habari na mitandao ya udaku kwa sababu mbalimbali, Gloria Bugie anaamini kuwa umaarufu hautabadilisha utu wake.
Katika mahojiano Bugie alieleza kuwa umaarufu hauwezi kumbadilisha na kwamba ataendelea kuwa mtu wa kawaida kama alivyo sasa.
“Sidhani kama umaarufu utanibadilisha sana. Nitaendelea kuwa mtu yuleyule. Hata kama mambo yanayokuzunguka yatabadilika, bado unabaki kuwa binadamu kama wengine wote, na siku moja utakufa. Kuna baadhi ya mambo, kama umaarufu, ambayo hayawezi kunibadilisha,” alisema.
Aidha, Bugie alifichua kuwa analinda amani yake ya moyo kwa kuepuka kuwa karibu sana na watu, akisema anaogopa kukatishwa tamaa na wale anaowazoea.
“Nina marafiki, lakini siweki ukaribu sana na watu. Nina urafiki na wengi, ninazungumza nao na kutabasamu nao, lakini siwaruhusu wanikaribie sana. Sijifungi kihisia kwa watu kwa sababu unaweza kuishia kukatishwa tamaa. Ni bora zaidi kuweka umbali fulani,” alieleza.
Gloria Bugie ambaye jina lake halisi ni Gloria Busingye alizaliwa Septemba 22, 1997 na ni mwanamuziki wa mitindo ya Afrobeat na Dancehall mwenye asili ya Rwanda anayeishi Kampala, Uganda.
Akisimamiwa na kampuni ya Hitboss Management, Gloria amejijengea jina kwa kasi na kuwa miongoni mwa sauti zinazotamba katika kizazi kipya cha muziki wa pop Afrika Mashariki.
Alianza kupata umaarufu mkubwa kupitia wimbo wake wa ‘Nyash’, unaojulikana pia kama ‘Bankyawa’.