Isaac Katende mtangazaji wa Uganda ambaye wengi wanamfahamu kama Kasuku, anataka wanamuziki Pallaso na King Saha pamoja na magenge yao wapigwe marufuku.
Ghadhabu ya Kasuku inatokana na ugomvi uliotokea katika eneo la burudani la Supremacy Lounge uliowaacha wengi wakiwa wamejeruhiwa Jumatano usiku.
Pallaso na King Saha walijikuta katika eneo moja huko Nakulabye wakati wa tamasha ya MC Scorpion, ambayo ilihudhuriwa na wasanii wengi maarufu akiwemo Spice Diana na Sqoop Larma.
Kutokana na historia ya kutokuelewana kwa muda mrefu, Pallaso na King Saha waliingia kwenye mzozo ambao, kulingana na mashuhuda, ulianzishwa na wanachama wa magenge yao husika.
Muda mfupi baadaye, vurugu zilizofuata ziliwaacha baadhi yao wakiwa wamejeruhiwa vibaya, huku mmoja wa walinzi wa Pallaso akikimbizwa hospitalini akiwa na jeraha kubwa mkononi.
Kasuku amesema kuwa hatua za haraka lazima zichukuliwe dhidi ya matukio kama hayo kwa sababu yamesababisha kuanguka kwa sehemu nyingi za starehe jijini.
Ameomba usimamizi wa Supremacy Lounge kuchukua hatua za haraka kwa kuwazuia wasanii hao wawili pamoja na magenge yao kuingia tena ukumbini humo, ili wateja wa kawaida waweze kuhisi usalama wanapokuwepo hapo.