Seneta wa Siaya Dkt. Oburu Oginga ameondoka katika hospitali moja jijini Nairobi ambako alikuwa amelazwa akipokea matibabu.
Maspika Moses Wetang’ula wa Bunge la Taifa na Amason Kingi wa Seneti waliwaongoza viongozi mbalimbali wa mabunge hayo kumtembelea Seneta Oburu katika makazi yake jijini Nairobi kumtakia nafuu ya haraka.

Seneta Oburu akitumia fursa hiyo kusisitiza umuhimu wa mazungumzo katika kuangazia changamoto zinazoikumba nchi hii.
“Uongozi wa kweli unatuhitaji wakati wote kutafuta maelewano, kukuza ustahimilivu wa kisiasa, na kuweka kipaumbele kwa maslahi ya nchi,” alisema Dkt. Oburu.
Kwa upande wake, Wetang’ula alimsihi Seneta huyo wa Siaya kutenga muda wa kutosha wa kupumzika na kupata nafuu kikamilifu.
“Nilimtia moyo (Dkt. Oburu Oginga) kutoa kipaumbele kwa afya yajke na kujipa muda wa kutosha kupona kikamilifu kabla ya kurejelea shughuli zake za kisiasa,” alisema Wetang’ula baada ya mkutano wao.
Spika Kingi akielezea jinsi walivyomkosa Seneta Oburu katika Seneti.
“Tulifurahi kumpata kinara wa ODM akiwa mchangamfu na akiendelea kupata nafuu vizuri. Tumlimtakia kwa dhati nafuu ya haraka, tukiahidi kuendelea kumwombea na kusimama naye katika kipindi hiki,” alisema Kingi.
“Katika Seneti, tumekosa sana michango ya thamani ya Dkt. Oburu kwa vikao vya Seneti, ushauri wake wa busara na umaizi wake katika masuala ya siasa za kitaifa.”
