Mpiga muziki wa Injili, Samuel Muraya, maarufu kama DJ Mo, alifikishwa mahakamani jijini Nairobi leo alasiri kujibu mashtaka yanayohusiana na makosa ya trafiki.
Haya yanatokana na tukio la asubuhi na mapema na maafisa wa polisi katika Barabara ya Thika.
Muraya alifikishwa mahakamani baada ya kudaiwa kusimamishwa na polisi majira ya saa mbili na dakika 55 asubuhi Novemba 4, 2026, karibu na eneo la Roasters, alipokuwa akiendesha gari lake aina ya Jaguar lenye nambari za usajili KCH 065T.
Upande wa mashtaka unadai kuwa Mo alikuwa akiendesha gari hilo bila kuwa na bima halali, kosa linalokiuka Sheria ya Bima ya Magari ya Watu Wengine.
Pia anakabiliwa na shtaka la pili la kudaiwa kutokuwa na cheti halali cha bima kilichopachikwa ndani ya gari hilo kama inavyotakiwa kisheria.
Shtaka la tatu linahusiana na madai ya kukaidi amri halali ya polisi.
Mahakama ilielezwa kuwa Koplo Chelimo, aliyekuwa amevalia sare za polisi, alimwamuru Muraya kupeleka gari hilo katika kituo cha polisi, lakini anadaiwa kukataa na badala yake kuendelea na safari kuelekea Thika.
Kosa hilo linahukumiwa chini ya Sheria ya Trafiki nchini Kenya.