Mwenyekiti wa chama cha upinzani nchini Tanzania CHADEMA, Tundu .A. Lissu, amejumuishwa kwenye orodha ya wawaniaji watatu wa Tuzo ya Sakharov ya Uhuru wa Mawazo ya mwaka 2026, inayotolewa na Bunge la Ulaya.
Kamati za Mambo ya Nje na Maendeleo za Bunge la Ulaya zimemchagua Lissu pamoja na wagombea wengine wawili ambao ni Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, ICC na dada mapacha kutoka Iran, Taraneh na Romina Rahimi.
Lissu, ambaye ni kiongozi mashuhuri wa kisiasa na amekabiliwa na kile kinachoelezwa kuwa ni mateso ya kisiasa kwa miaka kadhaa, ameteuliwa kutokana na msimamo wake thabiti katika kutetea haki za binadamu na uhuru wa kidemokrasia nchini Tanzania.
Anashindana na ICC, iliyoteuliwa kwa kazi yake ya kimataifa ya kuchunguza uhalifu wa kivita, pamoja na dada hao wa Iran wanaowakilisha watu wanaokabiliwa na mateso chini ya utawala wa Kiislamu nchini humo.
Tuzo ya Sakharov ni heshima ya juu zaidi inayotolewa na Umoja wa Ulaya kwa kutambua mchango katika utetezi wa haki za binadamu.
Mshindi wa tuzo hiyo kwa mwaka 2026 anatarajiwa kutangazwa rasmi na Bunge la Ulaya Oktoba 22, 2026.
Sherehe rasmi za kukabidhi tuzo hiyo imepangwa kufanyika mjini Strasbourg, Ufaransa, katika kikao cha Bunge la Ulaya cha mwezi Desemba.
Viongozi wa Afrika waliowahi kutunukiwa tuzo hiyo ni pamoja na Nelson Mandela Rais wa zamani wa Afrika Kusini, mwaka 1988, Hauwa Ibrahim, Mwanasheria wa haki za binadamu wa Nigeria mwaka 2005 na Denis Mukwege, daktari bingwa wa upasuaji wa magonjwa ya wanawake wa asili ya DRC mwaka 2014.