Mwigizaji wa Kenya William Okore, anayefahamika kwa jina la Onyi, kupitia kipindi maarufu cha televisheni cha The Real Househelps of Kawangware, ameanza rasmi mpango wa miezi mitatu wa kurekebisha hali.
Anahudhuria mpango huo katika Kituo cha NACADA cha Urekebishaji wa Tabia za Waraibu wa Mihadarati kilichopo Miritini, Mombasa.
Hatua hii imejiri siku chache baada ya mwigizaji huyo kutoa ombi la dhati la msaada hadharani, jambo lililozua mjadala mkubwa katika tasnia ya burudani nchini Kenya.
Mwigizaji huyo aliwahi kupata umaarufu mkubwa nchini na kuwa na hali nzuri ya kifedha, alipoanza kukumbwa na changamoto hizo, ilidhihirisha jinsi tasnia ya ubunifu ilivyo na misukosuko isiyotabirika.
Mwanamuziki na Mbunge wa zamani wa Starehe, Charles Njagua Kanyi, maarufu kama Jaguar, alishirikiana na Ofisi ya Ombudsman pamoja na Afisa Mkuu wa Kaunti ya Nairobi, Geoffrey Mosiria, kuhakikisha Onyi anapata msaada unaohitajika.
Jaguar, ambaye aliwahi kuwa mkurugenzi katika Mamlaka ya Kitaifa ya Kupambana na Matumizi Mabaya ya Pombe na Mihadarati, NACADA, aliwasiliana na maafisa husika ili kuhakikisha Onyi anapata nafasi katika kituo hicho.
Mpango huo haujajikita tu katika matibabu, bali pia kumsaidia mwigizaji huyo kurejea katika maisha ya kawaida, huku Jaguar akijitolea kugharamia mahitaji yake binafsi, kumnunulia bidhaa muhimu na kumtembelea mara kwa mara katika kipindi chote cha miezi mitatu.