Nyota wa muziki wa Taarabu nchini Tanzania Khadija Kopa amelalamikia kile anachoitaja kuwa kutofaidika na mfumo mzima wa utoaji wa mirabaha.
Alikuwa akizungumza jana katika kikao na wanahabari ambapo aliandamana na msanii mwenza Isha Mashauzi kutangaza ujio wa maadhimizho ya miaka 20 ya Mashauzi katika muziki.
Kopa ambaye pia anafahamika kama Malkia wa Mipasho, alisema licha ya kufanya muziki kwa zaidi ya miaka 40, bado hajafaidika ipasavyo na mfumo wa mirabaha, huku akisema bila usaidizi wa Serikali ni vigumu mziki huo ufike mbali.
Msanii huyo ambaye ni mama mzazi wa msanii Zuchu sasa anaomba Baraza la Sanaa la Taifa, BASATA kutoa msaada zaidi kwa wasanii wa muziki wa Taarab ili kuhakikisha wananufaika na kazi zao.
Alitetea wasanii wa kiume wa muziki wa taarabu ambao mara nyingi husingiziwa kuwa mashoga kwa sababu muziki huo huchukuliwa kuwa wa wanawake. Kulingana naye, wanaodhania wasanii wa kiume wa taarabu kuwa hivyo ndio wana matatizo.
Kwa upande mwingine, amewataka waandaaji wa tamasha ya miaka 30 ya Bongo Fleva kuwajumuisha pia wasani kutoka Zanzibar, akisisitiza kuwa Tanzania ni Nchi moja.
Kulingana naye, wasanii wa Taarabu hawakualikwa kwa tamasha hiyo ya mzunguko huku wasanii wa Bongo Fleva wa Zanzibar nao wakikosekana kwenye orodha ya watumbuizaji.