Isha Mashauzi kusherehekea miaka 20 katika muziki

Hafla hiyo itakuwa tarehe 24 mwezi Oktoba mwaka huu wa 2026 katika ukumbi wa Super Dome uliopo Masaki, Dar es Salaam.

Marion Bosire
2 Min Read

Msanii wa kike wa muziki wa Taarab nchini Tanzania, Isha Mashauzi, ametangaza ujio wa tamasha yake maalumu ya kusherehekea miaka 20 ya safari yake ya muziki.

Akizungumza katika kikao na wanahabari jana akiwa na msanii mwenza Khadija Kopa, Mashauzi alisema hafla hiyo itafanyika tarehe 24 mwezi Oktoba mwaka huu wa 2026 katika ukumbi wa Super Dome uliopo Masaki, Dar es Salaam.

Mashauzi aliahidi onyesho la kipekee siku hiyo kutoka kwake binafsi na wasanii mbalimbali wa Taarab na Bongo Fleva, akiwemo Khadija Kopa na Fid Q.

Msanii huyo ambaye jina lake halisi ni Isha Ramadhan aliwahi kutangaza ujio wa tamasha hiyo mwezi Juni ambapo alifaa kuiandaa mwezi Agosti lakini haikufanyika.

Alianza muziki mwaka 2006 na sasa tuko mwaka 2026 na kulingana naye, hilo sio jambo la kuacha lipite hivi hivi akiambia mashabiki wake wote kwamba malkia amerejea baada ya kimya cha muda.

Kimya hicho alisema kilichochewa na haja ya kuangazia zaidi biashara zake binafsi, hususan biashara ya chakula, lakini aliona ni wakati wa kurudi na kuendeleza mchango wake katika muziki wa taarabu.

Katika maandalizi ta tamasha hiyo, Isha Mashauzi ametoa kibao kipya kiitwacho “Kacheze Unakochezaga” na ni miongoni mwa nyimbo atakazoimba siku hiyo.

Tamasha hiyo itakuwa fursa ya kukutana tena na mashabiki wake, kukumbuka historia ya safari yake ya muziki na kuonyesha kuwa bado ana nafasi kubwa katika kuendeleza muziki wa taarabu nchini humo.

Share This Article