Upinzani wataka viongozi wanaohusishwa na vurugu za Migwena wakamatwe

Wamedai vurugu hizo zilichangia pakubwa aliyekuwa Rais Uhuru Kenyatta kukosa kuhudhuria makumbusho ya Raila Odinga.

Marion Bosire
2 Min Read

Viongozi wa muungano wa upinzani nchini Kenya sasa wanamtaka Inspekta Jenerali wa Polisi, Douglas Kanja, kutekeleza uchunguzi na kuwachukulia hatua za kisheria viongozi wa kisiasa wanaodaiwa kuhusika na vurugu zilizoshuhudiwa huko Migwena, Bondo, Kaunti ya Siaya, wakati wa maadhimisho ya mwaka mmoja tangu alipofariki Waziri Mkuu wa zamani, Raila Amolo Odinga.

Akizungumza na wanahabari huko Karen, Kaunti ya Nairobi, kiongozi wa chama cha Wiper, Kalonzo Musyoka, amemtaka mkuu huyo wa polisi kuimarisha uchunguzi dhidi ya washukiwa watano ambao tayari wamekamatwa na kuwachunguza viongozi wanaodaiwa kufadhili na kupanga vurugu hizo.

Kalonzo pia amedai kuwa tukio hilo lilichangia pakubwa aliyekuwa Rais Uhuru Kenyatta kukosa kuhudhuria maadhimisho hayo ya Alhamisi katika Kaunti ya Siaya.

Kiongozi huyo wa vuguvugu la upinzani la Ukombozi amewashutumu wanasiasa wanaounga mkono serikali kwa kuendeleza utamaduni wa kutumia makundi ya vijana kufanya vurugu.

Ameonya kuwa hali hiyo inachochea kutovumiliana kisiasa katika maeneo mbalimbali nchini, hasa dhidi ya viongozi wanaohusishwa na muungano wa upinzani.

Wakati huo huo, Kalonzo amekemea kile alichokitaja kuwa vitisho dhidi ya viongozi wa upinzani, akimtaja Gavana wa Trans Nzoia, George Natembeya, ambaye anadai kuwa walinzi wake wameondolewa na hivyo kumweka katika mazingira hatarishi.

Kalonzo amewataka Polisi kuhakikisha viongozi wa upinzani wanapatiwa ulinzi wa kutosha, akitaka usalama wake binafsi uhakikishwe kabla ya ziara yake ya eneo la Nyanza wiki ijayo.

Share This Article