Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Nairobi Davis Nathan Chelogoi, amepatikana na hati ya kuwalaghai watu watatu ardhi ya hekari 7.39 yenye thamani ya shilingi bilioni 1.35, katika eneo la Lower Kabete, kaunti ya Nairobi
Chelogoi alipatakana na makosa matano, ikiwa ni pamoja na udanganyifu, kughushi na kuwasilisha stakabadhi bandia.
Mahakama iligundua kwamba Chelogoi alighushi barua ya kukabidhiwa ardhi iliyokuwa na tarehe ya Januari 31, 1995, akisingizia kuwa stakabadhi hiyo ni halali iliyotolewa na Tume ya Ardhi Nchini.
Wakati huo huo, alipatikana na hatia ya kuwasilisha stakabadhi ghushi kwa Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai DCI mnamo Oktoba 11, 2023.
Upande wa mashtaka uliwasilisha ukiongozwa na Sonia Njoki, Hillary Isiaho na James Murage, uliwasilisha mashahidi 19 kwenye kesi hiyo iliyohusu ardhi iliyosajiliwa kama Nairobi/Block/80/44, iliyo katika eneo la Lower Kabete.
Hakimu Mkuu Dolphina Alego, alifutilia mbali dhamana ya Chelogoi na kutoa agizo kwamba azuiliwe katika gereza la Nairobi, akisubiri kutolewa hukumu yake Novemba 2, 2026.
Aidha, mahakama hiyo pia iliagiza kufutiliwa mbali kwa usajili wa ardhi au hatimiliki ya ardhi iliyotolewa kuhusu ardhi hiyo, na kuamua kwamba ardhi hiyo inamilikiwa na Ashok Rupshi Shah na Hitebkumar Amritlal Raja.