Naibu Rais Prof. Kithure Kindiki amewataka viongozi wa kisiasa wanaowania nyadhifa mbalimbali katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2027 kuendesha kampeni zao kwa amani na kuepuka matamshi ya uchochezi yanayoweza kuwagawanya Wakenya.
Akizungumza katika eneo bunge la Othaya, kaunti ya Nyeri, wakati wa ziara ya kukagua miradi inayotekelezwa na serikali kuu, Prof. Kindiki alionya kuwa siasa za migawanyiko na uchochezi zinaweza kuhatarisha usalama wa taifa na kudhoofisha mshikamano wa kitaifa.
Naibu Rais alisisitiza umuhimu wa viongozi kushindana kwa sera na hoja badala ya kutumia siasa zinazochochea uhasama miongoni mwa wananchi.
Wakati huo huo, Kindiki alitetea rekodi ya utendakazi wa serikali ya Rais William Ruto, akisema eneo la Mlima Kenya limepiga hatua kubwa za maendeleo chini ya utawala wa Kenya Kwanza.
Alitaja sekta za afya, miundombinu na nishati miongoni mwa maeneo ambayo serikali imewekeza katika juhudi za kuboresha maisha ya wananchi.
Kauli yake iliungwa mkono na Katibu katika Wizara ya Nishati, Alex Wachira, ambaye aliwahimiza wakazi wa Mlima Kenya kumuunga mkono Rais Ruto kwa muhula wa pili, akitaja miradi inayotekelezwa na serikali kama msingi wa kuendeleza ushirikiano huo.
Kwa upande wake, Mbunge wa Nyeri Mjini, Duncan Mathenge, ametoa wito wa juhudi za pamoja katika kukabiliana na utengenezaji na uuzaji wa pombe haramu, akisema biashara hiyo imeathiri vijana wengi katika eneo hilo.
Mathenge alisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya viongozi, vyombo vya usalama na jamii katika kukabiliana na janga hilo na kulinda mustakabali wa vijana.
Katika ziara hiyo, Naibu Rais aliandamana na viongozi mbalimbali, wakiwemo wabunge Wambugu Wainaina wa Othaya na Njoroge Wainaina wa Kieni, na Katibu katika Idara ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Caroline Karugu, miongoni mwa viongozi wengine.
Taarifa ya mwanahabari wetu William Khaemba