Navi Pillay, ametetea taasisi za haki za kimataifa na kujibu ukosoaji wa Rais wa Marekani, Donald Trump, akisema kipimo halisi cha haki ni maana yake kwa waathiriwa wa migogoro na ukatili.
Trump alielezea uamuzi uliofanyika mwaka huu wa Tuzo ya Amani ya Nobel kuwa ni wa “aibu” na “wa kuaibisha”, akisema kuwa hajawahi kumsikia mwanasheria huyo kutoka Afrika Kusini.
Katika mahojiano na BBC, Pillay, aliyewahi kuwa Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Binadamu, alitetea kazi yake na kuonya dhidi ya juhudi za kudhoofisha taasisi zinazolenga kuwawajibisha waliohusika na uhalifu mkubwa.
Akijibu ukosoaji wa Trump, Pillay aliwakumbusha watu walionusurika katika mauaji ya kimbari dhidi ya Watutsi nchini Rwanda mwaka 1994, ambao wengi wao walisubiri kwa miaka mingi kupata haki.
“Nadhani washauri wa kisheria wa Rais Trump wanapaswa kumweleza mambo haya yote na kumfahamisha umuhimu wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) katika kudumisha amani duniani,” alisema.
Pillay, ambaye aliwahi kuwa jaji katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, alizungumza wakati mahakama hiyo ikikabiliwa na shinikizo jipya kufuatia vikwazo vya Marekani.
Alisema anakusudia kuwatia moyo wafanyakazi wa mahakama hiyo na anaamini kuwa shinikizo hilo litakuwa la muda tu, kwa kuwa nchi wanachama zinaendelea kuunga mkono taasisi hiyo.
Pillay pia alitetea matokeo ya uchunguzi wa tume ya Umoja wa Mataifa aliyoiongoza, ambayo ilihitimisha kuwa mauaji ya kimbari yalikuwa yakitokea Gaza, madai yaliyokataliwa na Israel.
Alisema hitimisho la tume hiyo lilitokana na ushahidi uliothibitishwa na kusisitiza kuwa wachunguzi wanapaswa kuruhusiwa kuendelea na juhudi za kuwawajibisha wahusika bila kutishwa.
Kwa Pillay, Tuzo ya Amani ya Nobel haitambui tu mapambano yake ya miongo kadhaa dhidi ya ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini na kujitolea kwake kwa haki za kimataifa, bali pia umuhimu mpana wa kuwawajibisha waliohusika na uhalifu mkubwa.
Mshindi huyo wa tuzo ya mwaka 2026 alisema vijana kote barani Afrika wanampa matumaini, licha ya kile alichokitaja kuwa kuendelea kwa utawala wa kimabavu na ukandamizaji wa maandamano.
“Vijana ndio wanaonipa matumaini. Wanafahamu haki zao na wanadai mabadiliko. Wanaingia mitaani kuandamana. Wana haki ya kuandamana, lakini maandamano hayo yanakandamizwa,” alisema.
Pillay alisema yeye na wenzake wanataka kuongeza uelewa wa haki za binadamu miongoni mwa vijana wa Afrika na kuhamasisha kizazi kipya kupigania mabadiliko.
Pia alielezea wasiwasi wake kuhusu kutokuwa na usawa kwa wanawake, hususan katika nchi maskini na maeneo yenye migogoro, akisema anatumai kutumia mwangaza unaotokana na tuzo hiyo kuangazia suala hilo.
“Nimejizatiti kuangazia ukosefu wa usawa na kutokuwa kwa usawa kwa wanawake, hasa katika nyanja ya uchumi,” alieleza.
Pillay alisema kushirikisha watu maarifa kuhusu haki zao kunawawezesha kudai mabadiliko, somo ambalo anatumai litapata mwitikio kote Afrika na kwingineko duniani.
Taarifa ya BBC