Madereva wa mabasi Uganda watangaza mgomo wa kitaifa

Wanapinga masharti ya kusasisha beji za madereva na gharama za mafunzo ya kurejelea ujuzi wa udereva.

Marion Bosire
1 Min Read

Madereva wa mabasi nchini Uganda wametangaza mgomo wa kitaifa Kuanzia kesho Jumatatu, Oktoba 12, 2026.

Hatua hiyo huenda ikasababishia abiria wa mabasi kote nchini Uganda matatizo huku safari zikifutwa na nyingine kucheleweshwa kuanzia kesho.

Haya yanajiri baada ya Chama cha Madereva wa Mabasi nchini Uganda, UBDA kutangaza mgomo kupinga masharti ya kusasisha beji za madereva na gharama za mafunzo ya kurejelea ujuzi wa udereva.

Katika notisi ya Oktoba 8, 2026, UBDA iliwaelekeza wanachama wake kusitisha kuendesha mabasi hadi mamlaka husika zikutane na chama hicho na kutatua malalamishi yake.

Chama hicho kilielekeza notisi hiyo kwa umma na kunakili Chama cha Wamiliki wa Mabasi Uganda, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, pamoja na Kurugenzi ya Polisi wa Trafiki na Usalama Barabarani.

UBDA ilisema masharti ya kusasisha beji za madereva na gharama zinazohusiana na mafunzo yanaweka shinikizo la kifedha na kiutawala kwa madereva wa kitaalamu.

“Mpangilio wa sasa unawawekea madereva mzigo mkubwa wa kifedha, ilhali mishahara yao haitoshi kukidhi gharama za kila mwaka zinazojirudia,” sehemu ya notisi hiyo ilisoma.

Haya yanajiri wiki chache tu baada ya madereva wa mabasi kugoma katika nchi jirani ya Tanzania ambapo walikuwa akilalamikia mfumo ulioanzishwa na serikali wa alama kwa kila dereva.

Share This Article