Wasanii Uganda wakosolewa kwa kutoelewa sheria ya hakimiliki

Mwanzilishi Mwenza wa Swangz Avenue nchini Uganda, Julius Kyazze anasema tatizo sio uwepo wa sheria bali ni utekelezaji.

Marion Bosire
1 Min Read

Mwanzilishi Mwenza wa kampuni ya muziki ya Swangz Avenue nchini Uganda, Julius Kyazze amekosoa wasanii waliosherehekea kupitishwa kwa Sheria ya Hakimiliki ya Uganda.

Kyazze anasema wengi wao hawakuelewa matokeo yanayoweza kusababishwa na mabadiliko katika sheria hiyo.

Anasema furaha iliyozuka kufuatia marekebisho hayo haikuwa na msingi, akibainisha kuwa ingawa Uganda tayari ilikuwa na sheria ya hakimiliki, tatizo kubwa lilikuwa utekelezaji.

Kulingana na Kyazze, sheria iliyokuwepo ilihitaji kufanyiwa marekebisho ili iendane na mabadiliko ya nyakati, lakini akasema kuanzisha sheria mpya hakutaleta mafanikio makubwa iwapo mamlaka husika hazitatekeleza sheria hiyo.

Kwa mujibu wa mdau huyo wa tasnia ya muziki, mojawapo ya vipengele vilivyowafurahisha wasanii ni kupunguzwa kwa muda ambao mapato ya mirabaha huchukua kabla ya kurejeshwa kwa wamiliki wake wa awali, ikilinganishwa na kipindi kirefu kilichokuwepo chini ya sheria ya awali.

Hata hivyo, Kyazze alionya kuwa mabadiliko hayo yanaweza kuwa na matokeo yasiyotarajiwa katika biashara ya muziki, hasa kwa kuwakatisha tamaa wawekezaji wanaowekeza fedha katika utayarishaji na biashara ya muziki.

Kyazze anasisitiza kuwa utekelezaji madhubuti wa sheria zinazolinda hakimiliki ni muhimu, akidokeza kuwa mabadiliko ya sheria pekee hayawezi kutatua changamoto zinazoikabili tasnia ya muziki nchini Uganda ikiwa vifungu vilivyopo havitatekelezwa ipasavyo.

Share This Article