Mchekeshaji wa asili ya Uganda Yokana Mbuuse maarufu kama Kapere Lufotose amefariki.
Taarifa za kifo chake zilichapishwa kwenye mitandao ya kijamii na kiongozi wa chama cha upinzani NUP Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine.
“Muda mfupi uliopita, nilipokea taarifa za kusikitisha mno kuhusu kifo cha ghafla cha ndugu yetu, rafiki mpendwa na mwandani Yokana Mbuuse maarufu kama Kapere Lufotose,” aliandika Wine kwenye chapisho lake.
Aliendelea kumsifia mwendazake akisema kwamba alikuwa mtu aliyeleta mwangaza katika kila tatizo, mzalendo kamili wa Uganda aliyependa nchi yake na kuitakia mema.
Kiongozi wa Upinzani Bungeni nchini Uganda, Joel Ssenyonyi, naye aliomboleza kifo cha mchekeshaji huyo, akisema alikutana naye siku chache zilizopita.
“Wiki iliyopita tu, tulikuwa pamoja na Kapere Lufotose katika ofisi za NUP Kavule. Inasikitisha sana kusikia kwamba amefariki dunia. Kitalo nyo dala!” alisema Ssenyonyi.
Katika miaka ya hivi karibuni, Kapere amekuwa akihusishwa zaidi na upinzani, hasa chama cha NUP, na alikuwa akizungumzia waziwazi masuala ya kisiasa.
Kaimu Rais wa chama hicho cha upinzani, John Baptist Nambeshe, alimwelezea marehemu kama “mchekeshaji mwenye kipaji kikubwa ambaye talanta yake ilileta tabasamu, vicheko na furaha kwa Waganda wengi.”
“Alitumia ucheshi kama nyenzo yenye nguvu kuwasilisha ujumbe wa mabadiliko, matumaini na uelewa wa masuala ya kijamii. Alitukumbusha kwamba hata katika nyakati ngumu, kicheko kinaweza kuwapa watu nguvu na sababu ya kuendelea kuamini katika mustakabali bora,” alisema.