ODPP na UNODC zashirikiana kuwaelimisha watoto kuhusu haki zao

Wanafunzi hao walielimishwa kuhusu haki zao, makosa yanayohusishwa na teknolojia ibuka na jinsi ya kuripoti visa vya dhulma na kutafuta usaidizi.

Tom Mathinji
1 Min Read
ODPP na UNODC zashirikiana kuwaelimisha watoto kuhusu haki zao

Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ODPP), imeimarisha juhudi za kuwalinda watoto dhidi ya dhuluma za kimapenzi, ghasia za kijinsia na ukeketaji.

Huku ikishirikiana na afisi ya Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Mihadarati na Uhalifu (UNODC), afisi ya ODPP iliandaa vikao vya uhamasisho dhidi ya dhuluma hizo, katika shule ya msingi ya Wagberi na shule ya sekondari ya wasichana ya Wajir zilizo kaunti ya Wajir.

Wanafunzi hao walielimishwa kuhusu haki zao, makosa yanayohusishwa na teknolojia ibuka na jinsi ya kuripoti visa vya dhulma na kutafuta usaidizi.

Wawakilishi wa ofisi ya ODPP Leah Mati na Stellah Oyagi waliwahimiza watoto kuzungumza dhidi ya dhulma, wakisema kupiga ripoti mapema ni muhimu  katika kuwalinda waathiriwa na kuhakikisha wanaotekeleza dhulma hizo wanachukuliwa hatua.

“Ni sharti watoto wafahamu haki zao, watambue mbinu tofauti za dhuluma na wajue ni wapi watapata usaidizi,” alisema Oyagi.

Uhamasisho huo umewadia huku malalamishi yakiongezeka kuhusu usalama wa watoto mitandaoni.

Mitandao ya kijamii ilitambuliwa kuwa inayotumika sana kuendeleza dhulma hizo, huku visa vichache vya dhulma vikiripotiwa kwa maafisa wa utawala.

Share This Article