Rais William Ruto ametoa hakikisho kwamba Kenya imejiandaa vya kutosha kupambana na visa vya Ebola vinavyoweza kutokea.
Kufuatia kuwasili nchini na kufariki kwa Mkenya aliyeambukizwa ugonjwa huo kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, Ruto amesema serikali imechukua hatua za kuikinga nchi dhidi hatari zozote zinazotokana na kisa hicho.
“Tumechukua hatua za kuhakikisha tunailinda nchi,” alihakikisha Rais.
Aliongeza kuwa wale waliosafiri na mgonjwa huyo aliyefariki Jumatatu usiku, wahudumu wa afya waliomhudumia katika Nairobi Hospital na jamaa waliotangamana naye wametambuliwa na hatua mwafaka za afya ya umma kuchukuliwa.
Kiongozi wa nchi ametoa wito kwa Wakenya kuwa watulivu wakati serikali ikishughulikia suala hilo.
Alielezea kuwa Wizara ya Afya imetoa miongozo ya mienendo ya raia wanapokuwa maeneo ya umma ili kudhibiti hali hiyo.
“Katika saa na siku zijazo, tutaendelea kuiarifu nchi juu ya hatua muhimu zilizochukuliwa na serikali na zinazoendelea kuchukuliwa ili kuongeza uangalizi wetu hadi kiwango cha juu zaidi,” alisema Rais Ruto.
Alitoa hakikisho kuwa nchi ina vituo vya afya vya kutosha vinavyoweza kutumika panapokuwa haja.
Aliyasema hayo leo Jumatano wakati wa uzinduzi wa jengo la ukumbusho wa Hayati Raila Amolo Odinga huko Kang’o ka Jaramogi huko Bondo, kaunti ya Siaya.