Wito wa tahadhari zaidi dhidi ya Ebola wazidi kutolewa

Kenya imethibitisha kisa kimoja cha ugonjwa wa Ebola huku mgonjwa husika akiripotiwa kufariki baada ya kurejea nchini Jumamosi iliyopita akitokea DRC alikoishi kwa miaka 7.

Martin Mwanje
2 Min Read

Taasisi mbali zinazidi kutoa wito wa washikadau mbalimbali kuchukua hatua zaidi za kukabiliana na ugonjwa hatari wa Ebola unaosababishwa na virusi vya Bundibugyo. 

Kwenye taarifa, Chama cha Madaktari nchini Kenya, KMA kinasema ingawa kuthibitishwa kwa kisa kimoja ni suala nyeti, hamna haja ya kuhofu.

Kinatoa wito kwa umma na wahudumu wa afya kuchukua hatua mbalimbali za kuzuia ugonjwa huo ikiwa ni pamoja na kuwa waangalifu na kuripoti visa vya ugonjwa huo mapema punde mtu aliyetoka katika nchi za Jamhuri ya Demokrasia ya Congo, DRC, Uganda na Sudan Kusini siku 21 zilizopita anapoonyesha dalili za ugonjwa huo.

Dalili hizo ni pamoja na homa, udhaifu, kutapika, kuendesha na kuvuja damu kusikoelezeka.

Waliokuwa kwenye ndege ya Jambo Jet nambari ya usajili 8523 aliyosafiria mgonjwa wa kwanza na waliyetangamana naye pia wametakiwa kupiga ripoti mapema punde wanapoonyesha dalili za ugonjwa huo huku watu waliowekwa kwenye karantini wakitakiwa kufuatia maagizo kikamilifu.

“Tunatoa wito kwa serikali kuhakikisha vifaa vya kutosha vya kujikinga, PPE vinavifikia vituo vyote vya afya bila kukawia; kwamba vituo vya kujitenga wakati wote vinakuwa tayari, kwamba uangalizi katika maeneo ya kuingia nchini unaongezwa; na kwamba wahudumu wa afya walio kwenye mstari wa mbele wanakingwa na kusaidiwa,” alihimiza Dkt. Lyndah Kemunto, Katibu Mkuu wa KMA.

Chama cha Wafamasia nchini Kenya, PSK pia kimetoa wito sawia, kikiwataka wafamasia na timu zingine za kutoa huduma kuwa na uangalifu mkubwa katika utendaji kazi wao.

Kenya imethibitisha kisa kimoja cha ugonjwa wa Ebola huku mgonjwa husika akiripotiwa kufariki baada ya kurejea nchini Jumamosi iliyopita kutokea DRC. Mgonjwa huyo alipitia nchi jirani ya Uganda kabla ya kurejea nchini.

 

 

Share This Article