Maafisa 2 wa bunge la Nyamira wakamatwa kuhusiana na zabuni ya mamilioni

Martin Mwanje
1 Min Read
Maafisa waliokamatwa David Nyarango Ombego na Joyce Onyiego 

Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) imewakamata maafisa wawili zaidi wa bunge la Nyamira kuhusiana na madai ya utoaji zabuni wa shilingi milioni 367 bila kufuata sheria.

Zabuni hiyo ilikuwa ya ujenzi wa jengo la ofisi za bunge hilo.

Hatua hiyo yamkini ilisababisha kupotea kwa shilingi milioni 30.1 zikiwa pesa za umma.

Waliokamatwa ni David Nyarango Ombego ambaye ni Naibu Karani na Joyce Onyiego ambaye ni Mkurugenzi wa Ufuatiliaji na Tathmini.

Wote hao walikamatwa katika kaunti ya Kisii katika operesheni iliyoendeshwa na wapelelezi wa EACC.

Washukiwa wanatarajiwa kukabiliwa na mashtaka mbalimbali ikiwa ni pamoja na matumizi mabaya ya mamlaka na utepetevu katika utendaji kazi wao.

Wawili hao waliandikisha taarifa katika ofisi ya kanda ya South Nyanza wakisubiri kufikishwa mahakamani.

Maafisa wengine waliokamatwa awali kuhusiana na sakata hiyo ni Duke Simeon Onyari ambaye ni karani wa bunge la Nyamira; Mhandisi Josephat Matini Oruru ambaye ni afisa mkuu wa ujenzi wa barabara na kazi za umma na Simon Ondari Ogecha ambaye ni afisa wa miundombinu.

Share This Article