Shirika la Msalaba Mwekundu. limetangaza kuwa mwanamume ameokolewa kutoka kwenye vifusi vya jengo lililoporomoka Eastleigh, kaunti ya Nairobi.
Kulingana na Shirika hilo, mwanamume huyo aliyeokolewa leo Jumamosi anapokea huduma za matibabu katika Hospitali Kuu ya kitaifa ya Kenyatta (KNH), huku shughuli za kuwatafuta manusura wengine zikiendelea.
“Baada ya saa kadhaa za kuwatafuta manusura kwa ushirikiano na asasi zingine za dharura, maafisa wetu walimuokoa mwanamume aliyekuwa amekwama kwenye vifusi na anapokea matibabu katika hospitali ya Kenyatta,” ilisema taarifa ya Shirika la Msalaba Mwekundu.
Wakati huo huo, Shirika la Red Cross limesema kuwa wafanyakazi 66 kati ya 67 waliokuwa katika jengo hilo lililoporomoka wako salama, huku likitoa wito kwa wanaowatafuta wapendwa wao kufika kwenye kituo chao karibu na jengo hilo au kupiga nambari 1199 bila malipo.
Mashirika kadhaa ya serikali, yanashirikiana katika shughuli ya kuwaokoa waliokwama kwenye vifusi vya jengo hilo.