Mwanamitandao wa asili ya Tanzania anayeishi Kenya, Edger Edson Mwakabela maarufu kama Sativa255 ana kila sababu ya kutabasamu kufuatia kufutwa kwa hati iliyotolewa awali ya kumkamata na kumrejesha Tanzania.
Mahakama Kuu ya Tanzania ilitangaza uamuzi huo Septemba 29, 2026, ambapo Jaji Dafina Ndumbaro aliitangaza kuwa batili.
Jaji Ndumbaro aliafikia uamuzi huo baada ya hatua ya kusikilizwa kwa rufaa ya Sativa aliyoiwasilisha kupinga amri hiyo iliyotolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Jaji amesema hati ya kukamatwa kwake na maelekezo ya kutumia njia zote kumrejesha Sativa, anayeishi Kenya vimetangazwa kuwa batili, visivyo na nguvu na visivyo na athari yoyote kisheria.
Kwa mujibu wa Jaji Ndumbaro, mwenendo wa shauri katika mahakama ya chini ulifanyika kinyume na kifungu nambari 14(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, bila mamlaka ya kisheria chini ya Sheria ya Urejeshaji wa Watuhumiwa na kwa kutumia hati ya kiapo ya kuunga mkono shauri iliyokuwa na kasoro zisizoweza kurekebishika.
Sativa, kupitia wakili wake Jebra Kambole, alifungua rufaa dhidi ya uamuzi, mwenendo wa kesi na amri za Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu zilizotolewa Novemba 28, 2025, katika maombi ya jinai namba 28115 ya 2025.
Afisi ya mkurugenzi wa mashtaka ya umma nchini tanzania ndiye aliomba kutolewa kwa hati hiyo katika mahakama ya hakimu mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, kutokana na madai kwamba Sativa alichapisha taarifa za uongo mtandaoni.