Rubani ‘shujaa’ azuia janga angani baada ya kudungwa kisu na mwenzake

KBC Digital News
3 Min Read
Picha kwa hisani ya EPA

Rubani mmoja amekamatwa baada ya kumchoma kisu rubani mwenzake kwenye ndege iliyokuwa ikisafiri kutoka Dubai kwenda Tel Aviv na “inaonekana alijaribu kuiangusha ndege hiyo”, kwa mujibu wa Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu.

Abiria na wahudumu wa ndege walifanikiwa kumdhibiti mshambuliaji huyo na kurejesha udhibiti wa ndege ya shirika la Flydubai, ambayo baadaye ilitua salama katika uwanja wa ndege wa Tabuk, kaskazini-magharibi mwa Saudi Arabia, ikiwa na zaidi ya watu 170 ndani.

Abiria hao, ambao wengi wao walikuwa raia wa Israel, waliwasili baadaye Jumatano mjini Tel Aviv kwa ndege maalum ya kuwarejesha nyumbani.

Rubani aliyechomwa kisu, aliyetambulika kama raia wa India Kapteni Smit Machchhar, amelazwa hospitalini lakini hali yake inaelezwa kuwa imara.

Netanyahu pamoja na Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi, wamemsifu Kapteni Machchhar na kumtaja kama “shujaa” kutokana na mchango wake katika kusaidia kuzuia tukio hilo na kuokoa maisha ya watu waliokuwa ndani ya ndege.

“Licha ya kudungwa kisu na kujeruhiwa vibaya, alipambana, akajitetea, akafungua mlango wa chumba cha marubani na kuwawezesha abiria pamoja na wahudumu wa ndege kumdhibiti mshambuliaji huyo, na hivyo kuzuia janga kubwa ambalo lingeweza kutokea angani,” Netanyahu aliandika kwenye mtandao wa X.

“Aliokoa maisha ya watu 174, wakiwemo raia wa Israel na mataifa mengine.”

Ubalozi wa India nchini Saudi Arabia umesema Kapteni Smit Machchhar anaendelea kupatiwa matibabu hospitalini na hali yake ni thabiti.

Akitoa pongezi zake kwa rubani huyo, Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi, aliandika kwenye mtandao wa X: “Katika hali ya hatari kubwa sana, na licha ya kujeruhiwa vibaya, alionyesha ujasiri wa hali ya juu na azma isiyoyumba ya kulinda maisha ya wengine.”

“India inajivunia Kapteni Machchhar.”

Kauli hiyo ilikuja huku Kapteni Smit Machchhar akiendelea kupatiwa matibabu hospitalini baada ya kudungwa kisu akiwa kwenye ndege ya shirika la Flydubai iliyokuwa ikielekea Tel Aviv. Benjamin Netanyahu na Narendra Modi wamemsifu rubani huyo kwa kusaidia kuzuia kile walichosema kingegeuka janga kubwa angani

Sababu ya tukio hilo bado haijajulikana, na rubani anayeshukiwa alikuwapo chini ya uchunguzi wa mamlaka za Saudi Arabia, kwa mujibu wa Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu.

Akizungumza na kituo cha habari cha Fox News usiku wa Jumatano, Netanyahu alisema rubani huyo alitarajiwa kurejeshwa katika Falme za Kiarabu (UAE), ambako ndege hiyo ilianzia safari yake, baada ya taratibu za uchunguzi kukamilika.

Taarifa ya BBC

Share This Article