Wanandoa raia wa Tanzania wakamatwa kwa uhalifu Mombasa

Baada ya upekuzi kwenye nyumba ya washukiwa hao, DCI ilisema maafisa wa polisi walipata tarakilishi aina ya HP na simu aina ya iPhone 17 Pro Max za mwathiriwa.

Tom Mathinji
1 Min Read
Wanandoa raia wa Tanzania wakamatwa kwa madai ya kuhusika kwa uhalifu kaunti ya Mombasa.

Wanandoa raia wa Tanzania wanaodaiwa kuhusika kwenye uhalifu wa kuwawekea watu dawa za kuwapumbaza kabla ya kuwaibia, wamekatwa katika kaunti ya Mombasa.

Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), ilisema kisa cha hivi karibuni kilichowahusisha wanandoa hao kilinakiliwa Septemba 8, 2026, walipoabiri basi kutoka Nairobi kuelekea Mombasa, wakati walipomwekea abiria dawa za kumpumbaza na kumuibia mizigo yake.

“Maafisa wa Polisi kutoka kituo cha polisi cha makupa walianza uchunguzi mara moja, uchunguzi wao ukiwaelekeza eneo la Magongo na kumkamata Paskale Frugenze mwenye umri wa miaka 52 na mke wake Redempta Revelian Kuleta mwenye umri wa miaka 47, wote raia wa Tanzania,” ilisema DCI.

Baada ya upekuzi kwenye nyumba ya washukiwa hao, DCI ilisema maafisa wa polisi walipata tarakilishi aina ya HP na simu aina ya iPhone 17 Pro Max za mwathiriwa.

Wakati huo huo maafisa hao pia walipata simu kadhaa za mkononi, saa 10, nguo na bidhaa zingine zinazoaminika kuwa za wizi. Vile vile maafisa hao walinasa kile walichoshuku ni dawa za kuwapumbaza watu.

Wawili hao wanazuiliwa kwenye korokoro za polisi wakisubiri kufikishwa mahakamani.

Share This Article