Msanii wa muda mrefu wa mtindo wa Hip Hop nchini Tanzania, Stamina, amesema wasanii wakongwe bado wana mashiko.
Akizungumza katika kikao na wanahabari kuhusu kusajiliwa na kampuni ya Tala Waves, msanii huyo alisisitiza kwamba wakongwe bado wana nguvu kubwa ya kuvutia mashabiki.
Kulingana naye, wasanii wa kizazi cha sasa hawawezi kufikia uwezo wao wa kujaza ukumbi wa Mlimani City.
Akizungumza kuhusu mchango wa wasanii hao, Stamina alisema, “Wasanii 16 wa sasa ukiwaweka Mlimani City hawataweza kuujaza ukumbi, lakini hawa wakongwe wetu ni noma,”.
Stamina ambaye anatimiza miaka 16 katika tasnia ya muziki, alisema kwamba Watanzania wamepata zawadi kubwa kupitia kazi na mchango wao kwenye muziki.
Chini ya usimamizi wake mpya, msanii huyo ameahidi kazi nyingi mpya za sanaa pamoja na matamasha.
Kauli hiyo imeibua mjadala kuhusu nafasi ya wasanii wakongwe katika tasnia ya muziki na uwezo wao wa kuendelea kuvutia mashabiki licha ya kuibuka kwa kizazi kipya cha wasanii.
Huku haya yakijiri, tamasha ya kusherehekea miaka 30 ya muziki wa Bongo Fleva itaandaliwa Mwanza wikendi hii ambapo wasanii mbali mbali watatumbuiza.