Rais William Ruto na bilionea wa nchini Nigeria Aliko Dangote, leo Jumatano watazindua ujenzi wa kiwanda cha kusafisha mafuta katika kaunti ya Lamu.
Kiwanda hicho cha aina yake katika kanda ya Afrika Mashariki, kinatarajiwa kutengeneza bidhaa tofauti za petroli na zile za kutumiwa viwandani kwa soko za humu nchini na zile za Kimataifa.
Kulingana na bwanyenye huyo, kiwanda hicho kitasafisha mafuta ya ndege, dizeli na petroli huku kikisambaza mali ghafi kwa viwanda vya kutengeneza bidhaa za plastiki na watengenezaji bidhaa wengine.
Kwenye ukurasa wake wa X, Rais William Ruto alisema kiwanda hicho kitazalisha mapipa 700,000 ya mafuta kila siku kutokana na uwekezaji wa dola bilioni 16 za Marekani, sawa na shilingi trilioni mbili za Kenya.
Aidha, aliongeza kuwa kiwanda hicho kitafanikisha usalama wa nishati nchini Kenya na mataifa mengine nane ya Afrika Mashariki na kati, huku kikibuni nafasi 60,000 za ajira kwa vijana wa eneo hilo hilo.
Vile vile kiwanda hicho pia kitakuza sekta ya viwanda hasaa zile za mbolea, kemikali na upakiaji.
Hayo yanajiri wakati rais anaendelea na ziara yake katika eneo la Pwani iliyong’oa nanga Jumamosi iliyopita katika kaunti ya Taita Taveta.
Kiongozi huyo wa taifa anatarajiwa kuzindua na kukagua miradi ya maendeleo katika kauti za Kwale, Kilifi, Mombasa, Tana River na Lamu.