Wanne wapatikana na hatia mauaji ya Muchai

Erick Munyera Isabwa, Raphael Kimani Gacii, Mustafa Kimani Anyonyi, na Stephen Asitiva Lipapo wakipatikana na hatia kwa makosa manne ya mauaji.

Marion Bosire
4 Min Read

Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma, ODPP, imefanikisha kupatikana kwa hukumu ya hatia dhidi ya watu wanne waliomuua Mbunge wa zamani wa eneo la Kabete George Muchai, walinzi wake wawili na dereva.

Jaji Kanyi Kimondo wa Mahakama Kuu ya Milimani aliwapata na hatia Erick Munyera Isabwa, Raphael Kimani Gacii, Mustafa Kimani Anyonyi, na Stephen Asitiva Lipapo kwa makosa manne ya mauaji.

Watu hao wanne tayari wanatumikia vifungo vya kifo katika Gereza Kuu la Kamiti kwa kosa la wizi wa kimabavu.

Mahakama ilifahamishwa kwamba usiku wa tarehe 6 na 7 Februari 2015, kando ya barabara ya Kenyatta Avenue jijini Nairobi, kwa pamoja walimuua George Mukuru Muchai, na maafisa wa polisi Samuel Kimathi Kailikia, Samuel Lekakeny Matanta na Stephen Ituu Wambugu.

Washtakiwa hao wanne walipatikana na hatia baada ya Mahakama Kuu kubaini kwamba upande wa mashtaka ulikuwa umethibitisha kesi yake bila shaka yoyote kwa kuonyesha kwamba washtakiwa walitenda kwa nia na lengo la pamoja.

Upande wa mashtaka uliita mashahidi 37.

Miongoni mwa mashahidi ni Ronald Nyangaresi, muuzaji wa magazeti kwenye barabara ya Kenyatta Avenue, aliyesema kwamba usiku wa tukio, takribani saa tisa na dakika 40 alfajiri, gari lilisimama na Marehemu Muchai, aliyekuwa mteja wa kawaida kwa miaka 10, akaomba magazeti.

Alipokuwa akijiandaa kumpa baadhi ya magazeti, gari jingine lilizuia gari la Muchai kabla ya mtu aliyekuwa amevaa barakoa na kubeba bunduki aina ya G3 kutoka upande wa abiria wa mbele wa gari hilo. Kisha milio ya risasi ikasikika.

Mkewe Muchai, Susan Nyawira Muchai na dadake Judy Wanjiku Ngige, waliiambia mahakama kwamba walikuwa wakisafiria gari lililokuwa mbele ya gari la Muchai baada ya kuondoka eneo la burudani la Galileo Lounge huko Westlands.

Walisimama baada ya kugundua kuwa gari la Muchai lilikuwa limesimama na kusikia milio ya risasi. Walipofika, waliwakuta watu wote wanne waliokuwa ndani ya gari wamepigwa risasi, huku madirisha ya gari yakiwa yamevunjika.

Michael Ngatia Gituto alitoa ushahidi kwamba gari lake aina ya Nissan Sunny, lenye nambari ya usajili KBF 796A, lilitekwa kwa nguvu karibu saa 4 usiku wa tarehe 6 Februari 2015, kando ya Waiyaki Way na baadaye likatumika kulizuia gari la Muchai.

Gladys Waithera na dada yake Irene Wambui pia walisema kwamba walitekwa nyara wakiwa kwenye gari, wakafunikwa macho na kulazimishwa kuingia kwenye buti la gari lao.

Walisema gari hilo lilisimama mahali fulani na wakasikia milio minne au mitano ya risasi kabla ya kuachwa Kamandura karibu na Tigoni.

Mtaalamu wa uchunguzi wa balestiki Alex M. Mwadawiro na mchambuzi wa picha za CCTV, Inspekta Jackson Cheboi, pia walitoa ushahidi.

Inspekta Cheboi aliwasilisha picha za CCTV zilizokuwa na nambari 35 za magari yaliyorekodiwa karibu na Kenyatta Avenue.

Ripoti nne za uchunguzi wa miili zilizowasilishwa na Daktari Johansen Oduor zilionyesha kwamba waathiriwa walifariki kutokana na majeraha ya risasi yaliyosababishwa na silaha yenye kasi kubwa ya risasi iliyofyatuliwa kwa umbali wa karibu.

Mahakama imeamuru kwamba rekodi zao za awali zipatikane na kwamba Idara ya Urekebishaji Tabia (Probation Department) iandae ripoti za kabla ya hukumu pamoja na Taarifa za Athari kwa Waathiriwa.

Mahakama imepanga tarehe 16 Desemba 2026 kwa ajili ya kusikilizwa kwa hukumu ya adhabu, kesi hiyo iliendeshwa na mwendesha mashtaka Peris Maina.

Share This Article