Uongozi wa bendi tajika ya Uganda Afrigo, umehakikishia wateja, mashabiki na umma kwa jumla kwamba bendi hiyo itaendelea na shughuli zake.
Haya yanafuatia kifo cha mwanzilishi mwenza na kiongozi wake, Moses Matovu, maarufu kama Papa Moi.
Moses Matovu alifariki tarehe 24 Septemba 2026, baada ya zaidi ya miongo mitano akiwa mstari wa mbele katika kundi hilo la muziki la muda mrefu zaidi nchini Uganda.
Katika taarifa rasmi ya tarehe 28 Septemba, uongozi ulitoa shukrani kwa Serikali, Jeshi la Polisi la Uganda, wasanii wenza na umma kwa msaada walioutoa wakati wa maombolezo.
Uongozi huo ulisema kuwa maonyesho yote ambayo tayari walikuwa wamekubali kuhusika yataendelea kama ilivyopangwa, ukisisitiza uimara wa bendi na kujitolea kwake kudumisha ubora wa maonyesho ambayo Afrigo inajulikana kwayo.
Taarifa hiyo ilisema pia kwamba urithi wa marehemu Matovu, ukiwemo nidhamu, kipaji na maadili aliyoyajenga ndani ya bendi, utaendelea kuwa mwongozo katika shughuli za bendi.
“Afrigo Band itaendelea kuishi kwa heshima yake,” taarifa hiyo ilisema.
Wateja na washirika wanaohitaji huduma za bendi au kupata taarifa zaidi wameelekezwa kuwasiliana na Mkurugenzi Mtendaji James Wasula au Herman Ssewanyana.
Kwa zaidi ya miongo mitano, Matovu alihudumu kama kiongozi, mcheza ala mkuu na mwimbaji katika bendi ya Afrigo iliyobuniwa Novemba 1, 1975, na waimbaji waliogura bendi ya Cranes.