Rais William Ruto amesema uzinduzi wa ujenzi wa kiwanda cha kusafisha mafuta katika kaunti ya Lamu utaendelea kama ulivyopangwa.
Rais Ruto anatarajiwa kuongoza uzinduzi huo kesho Jumatano katika hafla itakayohudhuriwa na Marais kadhaa wa Afrika Mashariki.
“Kwa mapenzi ya Mungu Inshallah, kesho tunaanzisha refinery ya trilion mbili pale Lamu. Na mimi nataka niwaeleze ya kwamba hiyo refinery itabadilisha sehemu kubwa ya uchumi wa taifa letu,” alisema Rais Ruto wakati akipuuzilia mbali wale wanaojaribu kukimbilia mahakamani kupinga uzinduzi wa mradi huo.
“Kuna watu wanafikiri kwamba wanaweza kuhujumu investment ya hiyo refinery. Nimewaona wakijaribu maneno maneno, kule kwa mitandao, sijui kwa mapress conference, sijui wanasema nini, mimi nataka niwaambie hao watu, hamuwezi kututapeli siku zote, hamuwezi kutadanganya siku zote. Kwa sababu ya utapeli wenu, wale mabroker wa shares, wanatuambia sijui share, sijui wanataka share, utapeli huo mlioendesha ndio Kenya hii ikakosa uwekezaji.”
Akizungumza wakati akitoa hatimiliki za ardhi kwa wakazi wa Kilifi leo Jumanne, Rais Ruto alisikitikia miradi muhimu ambayo Kenya ilikosa siku zilizopita kwa sababu ya urasimu.
“Huyo huyo Dangote alikuwa aweke hapa kampuni ya simiti, alizungushwa hapa na mambo ya shares, alizungushwa hapa na mambo ya masharti, mpaka akaenda kwingine. Hapa hapa Kenya, tulikuwa na nchi ya Uganda, ilikuwa ijenge mfereji, pipeline ya crude ipitie hapa Mombasa. Hawa hawa matapeli wa shares na ukora, brokers wakazungusha nchi yetu jirani ya Uganda mpaka ile mfereji, pipeline ikapelekwa Tanzania.”
Kauli za Rais Ruto zinawadia siku moja baada ya baadhi ya wakazi wa Lamu kuelekea mahakamani kupinga uzinduzi wa kiwanda hicho hadi walipwe fidia la sivyo wapewe makazi mbadala.
Wanahoji namna ardhi yao ya ukoo inaweza kuchukuliwa kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda hicho kabla maslahi yao hayajatiliwa maanani.
Serikali ya Kenya Kwanza imetaja ujenzi wa kiwanda hicho kuwa mradi wa kupigiwa mfano utakaofungua uchumi wa eneo la Lamu na Pwani kwa jumla kwa kubuni takriban nafasi za ajira 50,000.