Mwimbaji wa nyimbo za Injili nchini Uganda, Gabie Ntaate amewajibu Wakristo wanaotilia shaka wokovu wake kwa sababu yeye ni Mwadventista wa Sabato.
Ntaate anasisitiza kwamba yeye ameokoka na imani yake imejikita kikamilifu katika Yesu Kristo.
Akizungumza katika hafla ya tuzo za VIGA, Ntaate alisema amekuwa akiulizwa mara kwa mara kuhusu imani na dhehebu lake, licha ya muziki wake wa injili kufikia Wakristo kutoka mashehebu mbalimbali.
“Wengi bado wanauliza kama nimeokoka,” alisema, kabla ya kujibu moja kwa moja, “Nitajisemea mwenyewe na kwa ajili ya Kristo ninayemtumikia. Nimeokoka.”
Ntaate alisema amechoshwa hasa na ukosoaji kuhusu utunzaji wake wa Jumamosi kama siku ya Sabato, akitetea imani ya Waadventista kwamba Sabato bado ni sehemu ya amri za Biblia.
“Basi niambieni, kwa nini tunateswa kwa kushika Sabato pekee iliyo katika Biblia?” aliuliza.
Mwimbaji huyo pia alipinga madai kwamba Waadventista wanahubiri ujumbe tofauti na Ukristo, akisema imani yake imejikita katika Biblia na Yesu Kristo.
Akitetetea imani yake, Ntaate alisema hawalaumu Wakristo wanaoabudu Jumapili, akimaliza kwa kuwaomba wanaomkosoa waache kuhoji imani yake, akisema hatashughulikia tena suala hilo.
“Niache,” alisema.