Msanii wa muziki wa Singeli wa asili ya Tanzania Meja Kunta ametoa taarifa baada ya mazishi ya mpendwa wake.
Kupitia mabango kwenye Instagram, Kunta alishukuru watu wote ambao walishiriki shughuli ya mazishi ya baba yake hiyo jana katika makaburi ya Kisutu, Jijini Dar es salaam.
Meja amesema ameguswa na upendo, msaada na faraja aliyopatiwa na ndugu, marafiki, mashabiki pamoja na wadau mbalimbali wa muziki nchini Tanzania katika kipindi kigumu cha msiba wake.
“Ndugu, marafiki na wote mlionisimamia, ninawashukuru kwa dhati kwa upendo, msaada na faraja mlionipa katika kipindi hiki kigumu cha kumpumzisha Baba yangu,” alisema katika ujumbe wake.
Aliendelea kutaja uwepo wao, michango waliyomtolea, sala zao na maneno ya kumtia moyo vitu ambavyo anasema kwamba vimenipa nguvu kubwa.
“Naomba Mwenyezi Mungu awalipie mema kwa kila jambo mlilonitendea, awazidishie afya, riziki na kuwalinda pamoja na familia zenu,” alimalizia Meja Kunta.
Mzee Mwarami Sadik Mtumbuka alifariki Jumanne Julai 21, 2026 baada ya kuugua akiwa na umri wa miaka 51.
Meja Kunta ambaye jina lake halisi ni Khalid Mtumbuka, anafahamika sana nchini Tanzania kwa muziki wake wa mtindo wa Singeli, akiwa ametoa nyimbo kama “Kinondoni” na “Wezi”.
Mzaliwa huyo wa Dar es Salaam, alianza muziki katika kundi lililofahamika kama ‘Team Jangwani’ kabla ya kuanza kuimba peke yake.