Baraza la Vyombo vya Habari Nchini (MCK), limetoa wito wa kuwepo kwa habari sahihi, za wakati na kuaminika, kabla ya kuandaliwa kwa Uchaguzi Mkuu mwaka 2027, likionya kuwa habari potovu huenda zikasababisha taharuki miongoni mwa jamii.
Mwenyekiti wa baraza hilo Maina Muiruri, amesema ukuaji wa majukwaa ya mtandao, umeibua changamoto mpya katika vita dhidi ya habari potovu, hususan kupitia mitandao ya kijamii.
“Majukwa ya dijitali yalibuniwa kutuunganisha pamoja, lakini pia yametoa fursa ya kuenezwa kwa habari potovu. Yanashinikiza yale ambayo tunafahamu badala ya kutoa changamoto na kile ambacho ni sahihi,” alisema Muiruri kwenye mkutano jijini Nairobi.
Aidha, mwenyekiti huyo alitoa wito kwa taasisi husika kuweka bayana habari ili kuwezesha wananchi ili kukabiliana na uenezaji wa habari ambazo sio sahihi.
Wakati huo huo, Muiruri aliwahimiza wadau kupanua fursa za upatikanaji wa habari, huku wakidumisha maadili.
“Tupanue upatikanaji wa habari, huku tukilinda maadili yetu,” aliongeza mwenyekiti huyo.