Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Uganda, Jenerali Muhoozi Kainerugaba, amesema kiongozi wa upinzani Robert Kyagulanyi Ssentamu, anayejulikana sana kama Bobi Wine, hataruhusiwa kugombea uchaguzi mwingine nchini Uganda.
Jenerali Kainerugaba, ambaye pia ni mshauri mkuu wa rais kuhusu operesheni maalum, alitoa kauli hiyo kwenye mtandao wa X, akimtaja kiongozi wa National Unity Platform, NUP kwa jina la “Kabobi”.
“Kabobi hataruhusiwa kamwe kugombea katika uchaguzi mwingine nchini Uganda tena,” alisema Jenerali Kainerugaba akiongeza kwamba Kyagulanyi ni kibaraka wa kigeni na akataja kuondoka kwake Uganda baada ya uchaguzi wa urais wa Januari.
“Alithibitisha kuwa ni kibaraka wa kigeni alipoondoka na kwenda nje ya nchi siku 10 baada ya uchaguzi uliopita. Hatutamruhusu tena yule mcheshi kugombea nafasi yoyote nchini Uganda. Kamwe!” aliongeza Mkuu huyo wa Majeshi.
Kyagulanyi aligombea urais katika uchaguzi wa mwaka 2021 na 2026.
Haya yanajiri wiki chache baada ya Jenerali Mohoozi kutangaza kwamba anapanga kuwania urais wa taifa hilo la Afrika Mashariki, katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2031.