Rais Ruto amwomboleza babake Martha Karua

Alimtaja kama mwalimu aliyejitolea na mtumishi wa umma aliyegusa maisha ya vizazi mbalimbali.

Marion Bosire
1 Min Read

Rais William Ruto ametuma salamu za pole kwa Waziri wa zamani wa Sheria, Martha Karua na familia yake kufuatia kifo cha babake, Mwalimu Jackson Karua.

Katika ujumbe aliouchapisha kwenye mitandao ya kijamii, Rais Ruto alisema amepokea kwa masikitiko makubwa habari za kifo cha Mwalimu Karua, akimtaja kama mwalimu aliyejitolea na mtumishi wa umma aliyegusa maisha ya vizazi mbalimbali.

“Mwalimu Karua alijitolea maisha yake katika ualimu na huduma, akigusa vizazi kupitia kazi yake na kuacha alama ya kudumu katika maisha ya watu wengi,” alisema Ruto.

Rais alitoa pole kwa kiongozi wa chama cha PLP Martha Karua, familia yake, jamaa na marafiki, akisema taifa linaungana nao katika kuomboleza msiba huo na kuheshimu maisha ya marehemu yaliyotumika katika huduma kwa jamii.

“Fikra na sala zetu ziko pamoja na familia katika kipindi hiki kigumu,” alisema Ruto.

Rais Ruto aliomba Mungu aipe familia iliyofiwa nguvu na faraja wakati huu wa majonzi, na kuomba roho ya Mwalimu Jackson Karua ipumzike kwa amani ya milele.

Martha Karua alitangaza kifo cha babake jana jioni, akielezea kwamba kilitokea mapema Jumapili, muda mfupi baada yake na ndugu zake kumtembelea.

Share This Article