Trump akataa mpango wa Iran wa kufungua Hormuz

Anasema kuwa Iran inataka makubaliano kwa sababu inashindwa vibaya sana.

Marion Bosire
2 Min Read
Donald Trump - Rais wa Marekani

Rais wa Marekani Donald Trump amekataa mpango uliowasilishwa na Iran wa kufungua Mlango wa Hormuz ndani ya wiki moja.

“Ninakataa pendekezo lao,” Trump aliambia waandishi wa habari nje ya Ikulu ya White House Jumamosi, akiongeza kuwa Iran inataka makubaliano kwa sababu inapoteza vibaya sana.

Kiongozi huyo alisema Iran inataka kuafikia makubaliano ambayo anadhani ni jambo zuri, akiongeza kwamba yeye pia anataka kuafikia makubaliano, ila anajua hayatakubalika.

Baada ya kauli za Trump, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araghchi alisema Iran imeona “mwitikio wa awali” kutoka kwa rais wa Marekani kuhusu pendekezo lake, lakini bado haijapokea jibu rasmi kupitia wapatanishi.

Tehran inasubiri wapatanishi kuwasilisha msimamo “wa mwisho” wa Washington kabla ya kuamua hatua inayofuata, Araghchi aliliambia shirika la habari la Iran IRNA.

“Suluhisho la mazungumzo pekee ndilo linaloweza kuwatoa katika mkwamo huu. Huo ndio msimamo wetu,” aliongeza.

Waziri huyo aliongeza kusema kwamba vigezo vyao viko waz na hatua yoyote ya kuelekea kufungua tena Mlango wa Hormuz inategemea kutimizwa kwa masharti hayo.

Araghchi alisema Ijumaa kwamba Tehran iliwasilisha rasmi kwa Marekani mpango wa hatua wa siku saba kupitia Qatar kama mpatanishi na ilikuwa ikisubiri jibu kutoka Washington.

Mwishoni mwa Ijumaa, ripoti za vyombo vya habari vya Marekani zilieleza kuwa Trump angekataa pendekezo hilo.

Share This Article