Marya kutumbuiza katika tamasha ya Mustafa

Mustafa ameelezea kuungana tena na Marya kama tukio la kipekee.

Marion Bosire
2 Min Read

Msanii wa muziki nchini Kenya, Colonel Mustafa, ametangaza kwamba msanii mwenza Marya atatumbuiza kwenye tamasha yake ya Oktoba 10, 2026.

Mustapha anatarajia kuadhimisha hatua muhimu katika safari yake ya muziki kupitia tamasha hiyo maalum.

Mustafa ametangaza kuwa Marya, ambaye amemtaja kama “mmoja wa wanawake wenye nguvu zaidi” kuwahi kuwa sehemu ya maisha yake, atapanda jukwaani katika hafla hiyo itakayofanyika ndani ya Imperial Chambers Lounge, kando ya Barabara ya Kiambu.

Tamasha hiyo inatarajiwa kuanza saa 1 usiku na itawakutanisha wasanii mbalimbali wa Kenya na kimataifa, akiwemo Nazizi, Mr. Nice, Kenrazy, Willy M Tuva, Kenzo Matata, J.I aliyeimba Kidato Kimoja na Marya, miongoni mwa wengine.

Hafla hiyo pia itakuwa na burudani kutoka kwa wapiga muziki DJ Extreme, Tatuah na Crucial, huku MC Dykes Global na MC Wilko254 wakiongoza shughuli za jukwaani.

Akizungumzia ujio wa Marya katika hafla hiyo, Mustafa alielezea muungano huo kama tukio la kipekee, akiandika, “Tumekutanishwa tena na ni hisia nzuri sana!” Aliongeza kuwa anatazamia kuwapa mashabiki onyesho la kukumbuka.

Mustafa amewahimiza mashabiki kujitokeza kwa wingi kushuhudia kile anachokieleza kuwa sherehe ya safari yake katika tasnia ya muziki. Ujio wa Marya jukwaani unaongeza ladha ya muungano katika usiku huo unaotarajiwa kuwa wa kipekee.

Marya na Mustafa waliwahi kushirikiana kikazi ambapo walitoa kibao kiitwacho “Hey Baby” cha mwaka 2009.

Share This Article