Ruto aanza ziara ya siku nane ya maendeleo Pwani

Ziara hiyo iliyoanzia Taita-Taveta, itampeleka Rais katika kaunti sita ambazo ni Taita-Taveta, Kwale, Kilifi, Mombasa, Tana River na Lamu.

Marion Bosire
1 Min Read

Rais William Ruto ameanza ziara ya siku nane ya maendeleo katika eneo la Pwani ya Kenya, huku umiliki wa ardhi, miundombinu na miradi ya nishati ikiwa miongoni mwa masuala muhimu katika mpango wake.

Ziara hiyo iliyoanzia Taita-Taveta, itampeleka Rais katika kaunti sita ambazo ni Taita-Taveta, Kwale, Kilifi, Mombasa, Tana River na Lamu.

Mojawapo ya mambo muhimu katika ziara hiyo ni ugawaji wa takribani hati miliki 190,000 kwa wakazi wa eneo hilo.

Hati hizo zinatarajiwa kuimarisha umiliki wa ardhi na kusaidia kutatua changamoto za muda mrefu zinazowakabili wananchi ambao hawana umiliki rasmi wa ardhi.

Huko Taita-Taveta, Ruto alikabidhi hati miliki na kuzindua ujenzi wa mabweni ya wanafunzi katika Chuo cha Ufundi na Mafunzo ya Kitaaluma cha Wumingu.

Mradi huo unatarajiwa kuongeza nafasi za malazi na kusaidia chuo hicho kukua.

Rais pia anatarajiwa kutembea Lamu, ambako ujenzi wa kiwanda kinachopendekezwa cha kusafisha mafuta cha Afrika Mashariki unatarajiwa kuzinduliwa.

Mradi huo unaokadiriwa kugharimu takribani Shilingi Trilioni 2, umepangwa kuwa uwekezaji mkubwa katika sekta ya nishati.

Wakati wa ziara hiyo, Ruto anatarajiwa kukagua miradi inayoendelea, kuzindua rasmi miradi iliyokamilika na kukutana na wakazi pamoja na viongozi wa eneo hilo kujadili vipaumbele vya maendeleo.

Share This Article