Wafanyabiashara waliowasilisha bidhaa na huduma katika serikali ya kaunti ya Kilifi, huenda watasubiri kwa muda zaidi kabla ya kupokea malipo yao yanayodaiwa kuwa takriban kitita cha shilingi bilioni 11.9.
Kwenye mkutano na maafisa wa serikali ya kaunti ya Kilifi, kamati ya Bunge la Senate kuhusu Uhasibu wa Pesa za Umma, ililalamika kuwa serikali ya Kilifi imeshindwa kubainisha kiasi halisi cha fedha kinachopaswa kuwalipa wafanyabiashara hao.
Mwenyekiti wa kamati hiyo Moses Kajwang’, alisema serikali ya Kilifi imetoa viwango tofauti vya malipo, huku maafisa wa kaunti wakisema mchakato wa kuthibitisha malipo halisi unaendelea.
Gavana wa Kilifi Gideon Mung’aro hata hivyo hakufika mbele ya kamati hiyo, lakini aliwakilishwa na naibu wake Flora Chibuhe, aliyeshindwa kuthibitisha ikiwa mchakato wa kubaini malipo ya wafanyabiashara hao unaendelea.
Ukosefu wa kiwango halisi cha malipo, umesababisha wafanyabiashara hao kuwa na wasiwasi wa ni lini watapokea malipo yao na kiwango cha malipo watakachopokea.
Bunge la Senate limeandaa vikao vya mikutano yake katika kaunti ya Kilifi, almaarufu Senate Mashinani, kwa lengo la kuwafikia wananchi na kutambua changamoto zinazowakabili.