Waliochochea ukuaji wa Kilifi watambuliwa na Senate

Wakazi hao walitambuliwa kutokana na michango yao ya kupigiwa mfano katika sekta za Utumishi wa Umma, jeshi, utamaduni, huduma za afya, masomo na michezo.

Tom Mathinji
4 Min Read
Amason Kingi - Spika wa Bunge la Senate.

Bunge la Senate Leo Jumatano limewatambua baadhi ya watu mashuhuri, ambao michango yao ilifanikisha ukuaji wa kaunti ya Kilifi.

Wakazi hao walitambuliwa kutokana na michango yao ya kupigiwa mfano katika sekta za Utumishi wa Umma, jeshi, utamaduni, huduma za afya, masomo na michezo.

Spika Amason Kingi aliongoza shughuli hiyo ya kuwatambua watu hao, iliyoandaliwa kwenye siku ya pili ya vikao vya Bunge la Senate katika kaunti ya Kilifi, katika mpango wake wa kila mwaka wa Senate Mashinani.

Kingi alielezea changamoto iliyoshuhudiwa kwenye mchakato wa kuwatambua watu hao, kutoka kwa orodha ndefu ya watu waliotoa mchango wa kupigiwa mfano katika kaunti hiyo nambari 003.

Miongoni mwa waliotambuliwa ni Timothy Chokwe, ambaye ndiye Spika wa kwanza wa Bunge la Senate aliyehudumu kati ya mwaka 1963 na 1966. Chokwe ni waziri wa zamani wa Ujenzi na Mawasiliano, mwanzilishi wa chama cha Kenya African Union na mpiganiaji wa uhuru wa Kenya.

Bunge hilo pia liliwatambua wabunge na mawaziri wa zamani Noah Katana Ngala, Samuel Kazungu Kambi, marehemu Emmanuel Karisa Maitha, marehemu Ronald Gideon Ngala na marehemu Robert Stanley Matano.

Matano alihudumu wadhifa wa mbunge wa eneo bunge la Kinango na Katibu Mkuu wa chama cha Kenya African National Union (KANU), pamoja na nyadhifa zingine katika Baraza la Mawaziri.

Aliyekuwa waziri na mbunge wa Malindi Aisha Jumwa Karisa Katana, pia alijumuishwa kwenye orodha hiyo.

Mchango wa Kilifi katika Vikosi vya Ulinzi uliwakilishwa na Jenerali Mstaafu Samson Jefwa Mwathethe, aliyekuwa Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi na Jenerali Mstaafu  Joseph Raymond Edward Kibwana, aliyekuwa Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi kati ya mwaka 2000 hadi 2005.

Meja Jenerali Mstaafu William Karisa Shume, aliyekuwa naibu kamanda wa jeshi la nchi kavu pia alitambuliwa.

Watumishi wengine wa umma waliotambuliwa ni pamoja na CPA Stephen Masha Ngowa, CBS, naibu mdhibiti wa bajeti, Katibu wa idara ya vijana Fikirini Jacobs na mwenzake wa sayansi, utafiti na uvumbuzi Prof. Shaukat Abdulrazak.

Katika sekta ya elimu waliotambuliwa wanajumuisha Prof. James H.P. Kahindi, naibu chansela wa Chuo Kikuu cha Pwani, marehemu Prof. Stephen Karisa Beja, na  Prof. Rocha Mzungu Chimera, profesa wa Swahili na kiongozi wa kitengo cha idara ya sayansi ya jamii katika Chuo kikuu cha Pwani.

Waliotambuliwa katika sekta ya afya ni Dkt. Mahfudh Muhammed, mwanzilishi wa hospitali ya Khairat na wakfu wa Khairat Medical Foundation, kutokana na mchango wake wa kutoa huduma za afya kwa bei nafuu kwa wakazi wa Kilifi.

Katika sekta ya sanaa na utamaduni waliotambuliwa ni bendi ya Them Mushrooms, inayotambuliwa kimataifa kwa wimbo maarufu wa Jambo Bwana, na marehemu  Fundi Konde, aliyetambuliwa kwa wimbo  Tausi Ndege Wangu.

Waliotambuliwa michezoni ni Mwanahalima Adam, nahodha wa timu ya taifa ya soka ya wanawake, Harambee Starlets, aliyekuwa mlindalango wa Harambee Stars Mohammed Salim Magogo, aliyewakilisha Kenya kati ya mwaka 1973 na 1977. Wengine ni aliyekuwa mshambulizi wa Harambee Stars Esse Mbeyu Akida, na marehemu Abbas Khamis Magongo.

Aidha, mpiganiaji wa uhuru wa Kenya Mekatilili wa Menza, pia alitambuliwa kwa kuongoza jamii ya wa Giriama dhidi ya ukoloni wa Waingereza katika karne ya 20, huku akichochea jamii hiyo kupinga sera za wakoloni, ikiwa ni pamoja na ushuru, kazi za lazima na mwingilio wa shughuli za kiuchumi za jamii hiyo.

Huku majina hayo yakisomwa, Maseneta walisimama kwa heshima kuyapokea kwa niaba ya taifa.

Hata hivyo, Spika Kingi alikariri kuwa orodha hiyo bado sio kamili, kwani kaunti ya Kilifi ina watu wengi ambao huduma zao zinatimiza uwezo wa kutambuliwa.

Share This Article