Spice Diana achagua hoteli ya Marriott Nsambya kwa tamasha yake

Alitangaza hayo kupitia akaunti zake za mitandao ya kijamii.

Marion Bosire
2 Min Read

Mwimbaji wa Uganda Spice Diana amechagua hoteli ya Marriot iliyoko eneo la Nsambya kuwa eneo la kuandaa tamasha yake ijayo.

Mrembo huyo alitangaza hayo kupitia akaunti zake za mitandao ya kijamii akiongeza tarehe ya hafla hiyo ambayo ni Januari 16, 2027.

Tamasha za binti huyo mara nyingi kufanyika mwanzo wa mwaka kama ile alitoandaa katika uwanja wa Lugogo Cricket Oval mnamo Januari 2023, hafla iliyozua minong’ono katika tasnia ya burudani nchini Uganda.

Pia aliwahi kusherehekea miaka yake 10 katika tasnia ya muziki kwa tamasha kubwa ya moja kwa moja iliyofanyika kwenye hoteli ya Serena jijini Kampala.

Spice Diana, ambaye jina lake halisi ni Namukwaya Hajara Diana, alipata umaarufu mwaka 2014 kupitia wimbo wake wa uitwao, Onsanula.

Tangu wakati huo, amejenga taaluma yenye mafanikio kupitia nyimbo kama Anti Kale, Now, Omusheshe, Kononya na Siri Regular.

Ameshinda tuzo mbalimbali, ikiwemo ile ya Msanii Bora wa Kike wa Mwaka katika tuzo za Zzina na Msanii Bora wa Kike Aliye na Mtindo Bora, katika tuzo za mitindo ya mavazi za Abryanz Style and Fashion.

Mbali na muziki, Spice Diana anajihusisha kwa kiasi kikubwa na shughuli za kusaidia jamii, akifadhili taasisi zinazosaidia watoto wenye mahitaji maalum na kutoa msaada kwa wahamiaji wa Uganda wanaokwama katika nchi za kigeni.

Share This Article