Mamake Sharon amwombea Obado kifungo cha nje

Alisema Sharon aliacha watoto na akaomba Obado apewe adhabu itakayomruhusu kusaidia familia kuwalea.

Marion Bosire
2 Min Read
Aliyekuwa Gavana wa Migori Okoth Obado.

Mamake mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Rongo aliyeuawa, Sharon Otieno, ameiomba mahakama izingatie kumpa aliyekuwa Gavana wa Migori, Okoth Obado, adhabu isiyohusisha kifungo gerezani.

Mama huyo Melinda Auma, alisema kwamba familia imemsamehe baada yake kuonyesha majuto na kuomba msamaha.

Melinda Auma aliambia mahakama wakati wa kusikilizwa kwa hoja za kupunguziwa adhabu kwamba uhusiano wa Obado na binti yake ulimfanya ashindwe kumtakia hukumu ya kifo au kifungo cha maisha.

Alisema Sharon aliacha watoto watatu ambao amekuwa akijitahidi kuwalea, na akaomba Obado apewe adhabu ambayo itamruhusu kusaidia familia katika kulea watoto hao.

Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma, ODPP ilitambua taarifa za waathiriwa pamoja na hati za kiapo kutoka kwa wazazi wa Sharon za kutafuta maridhiano, lakini ikasema maoni yao hayafai kuamua adhabu itakayotolewa.

Upande wa mashtaka ulisema kosa hilo linahusu serikali na jamii, na kwamba adhabu inapaswa kuimarisha imani ya umma katika haki, huku ukisisitiza kuwa mahakama ndiyo yenye uamuzi wa mwisho.

Baba ya Sharon, Douglas Otieno, alitofautisha mwenendo wa Obado na washtakiwa wenzake Michael Oyamo na Caspal Obiero, ambao aliwatuhumu kwa kutoonyesha majuto.

Alieleza hasira kubwa dhidi ya wawili hao, akisema walikuwa miongoni mwa watu wa mwisho kukutana na binti yake.

Jaji Cecilia Githua alisema mahakama itazingatia nyenzo zote zilizowasilishwa pamoja na hoja za maandishi za kupunguziwa adhabu kabla ya kutoa hukumu Novemba 27, 2026, saa 4:30 asubuhi.

Share This Article