Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta, KNH imetangaza kifo cha mtoto wa tano kati pacha watano waliopelekwa hospitalini humo kutoka Hospitali ya Thika Level Five kwa ajili ya kupata huduma maalum za kiwango cha juu.
Katika taarifa iliyotolewa leo Jumatano, Septemba 16, 2026, KNH ilisema watoto hao walizaliwa kabla ya wakati, ujauzito ukiwa wa wiki 25, hali iliyowafanya kuwa wadogo na wenye uzani mdogo sana wakati wa kuzaliwa.
Hospitali hiyo ilisema wahudumu na wataalamu wa huduma za watoto wachanga, wakiwemo madaktari bingwa wa watoto wachanga, wauguzi na wataalamu wengine wa afya, walitoa huduma maalum na kufanya kila juhudi kuokoa watoto hao.
Hata hivyo, licha ya juhudi za madaktari na huduma maalum walizopatiwa, watoto wote watano walifariki dunia.
“KNH imehuzunishwa sana na msiba huu mkubwa,” hospitali hiyo ilisema, huku ikitoa pole za dhati kwa mama na familia nzima.
Hospitali hiyo ilitambua maumivu makubwa yanayosababishwa na kumpoteza mtoto mchanga, na zaidi kwa familia iliyopoteza watoto watano kwa wakati mmoja. KNH ilisema iko pamoja na familia katika kipindi hiki kigumu sana.
Taarifa hiyo ilitiwa saini na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa KNH, Dkt Joel Lessan, OGW.
Kifo cha watoto hao kinaangazia changamoto kubwa za kitabibu zinazohusishwa na uzazi wa watoto wanaozaliwa kabla ya wakati, hasa wenye uzani wa kiwango cha chini na wanaohitaji huduma maalum na uangalizi wa karibu wa watoto wachanga.