Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, nchini Tanzania Paul Makonda, ameanza ziara maalum ya siku nne katika klabu ya FC Barcelona nchini Uhispania kwa mwaliko wa Rais wa klabu hiyo, Joan Laporta.
Makonda alianza ziara hiyo Jumatatu, Septemba 14, 2026, kwa kufanya mazungumzo na uongozi wa Barcelona kuhusu fursa za ushirikiano katika kuendeleza soka nchini Tanzania.
Mazungumzo hayo yalijikita katika maeneo mbalimbali, yakiwemo kukuza vipaji vya vijana, maendeleo ya kiufundi, uendeshaji wa timu ya taifa na namna uzoefu wa Barcelona unaweza kusaidia Tanzania katika maandalizi ya Kombe la Mataifa ya Afrika, AFCON mwaka 2027.
Kenya, Tanzania na Uganda, zitaandaa kwa pamoja mashindano hayo ya AFCON kuanzia Juni 19 hadi Julai 17, 2027.
Ziara hiyo inalenga pia kutafuta fursa za Tanzania kunufaika na uzoefu na mifumo ya Barcelona katika maendeleo ya soka.
Katika mazungumzo hayo, Laporta pia alimpa Makonda salamu za pole kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kufuatia kifo cha mume wake, Mzee Hafidh Ameir Hassan, kilichotokea Septemba 7, 2026.