Katibu wa Idara ya Utangazaji na Mawasiliano Stephen Isaboke amesema serikali imeweka mikakati ya kutosha ya kukabiliana na mvua ya El Niño, inayotarajiwa nchini Kenya kuanzia mwezi Oktoba hadi Disemba mwaka huu.
Idara kadhaa za serikali zimeshirikiana kwenya maandalizi hayo huku Kamati ya Kitaifa ya Kukabiliana na Majanga (NCCSC) ikitoa taratibu, mwongozo na kuandaa jinsi ya kuwasilisha jumbe kwa raia kabla, wakati na baada ya mikasa.
Jumbe hizo zinalenga kuwasaidia Wakenya kuchukua tahadhari ifaayo na kuchukua uamuzi mwafaka.
Idara ya Utabiri wa Hali ya Hewa nchini imetabiri kutokea kwa mvua kubwa nchini katika miezi ya Oktoba, Novemba na Disemba mwaka huu.
Viwango vya mvua katika maeneo mengi humu nchini vinatarajiwa kupita viwango vya wastani.
Hata hivyo, Isaboke amewataka Wakenya kutokuwa na hofu na badala yake kujiandaa ipasavyo kukabiliana mikasa ya mafuriko.
Aidha, NCCSC inajukumiwa na kutoa ripoti za mara kwa mara kwa umma kupitia kwa vyombo vya habari, kuhakikisha habari zifaazo zimefikia wananchi.
Kamati hiyo pia inamshirikisha Msemaji wa Serikali Charles Owino,
Pia kamati hiyo itaandaa jumbe za kuhamasisha umma kuhusu mvua na mafuriko na mbinu za kuchukua tahadhari kuzuia maafa na hasara.