Kongamano la Usafiri wa Anga: Mudavadi ahimiza ufunguzi wa anga za Afrika

Amesema kuimarisha muunganisho wa usafiri wa anga kutasaidia kuharakisha mabadiliko ya kiuchumi barani humu.

Marion Bosire
2 Min Read

Mkuu wa mawaziri nchini Kenya Musalia Mudavadi ametoa wito kwa nchi za Afrika kufungua zaidi anga zao, akisema kuimarisha muunganisho wa usafiri wa anga kutasaidia kuharakisha mabadiliko ya kiuchumi barani humu.

Mudavadi alitoa kauli hiyo baada ya kufungua rasmi awamu ya 10 ya kongamano na maonyesho ya usafiri wa anga almaarufu Aviation Africa Summit and Exhibition jijini Nairobi.

Mkutano huo umewaleta pamoja watunga sera, wawekezaji, wabunifu na viongozi wa sekta ya usafiri wa anga kujadili mustakabali wa sekta hiyo barani Afrika.

Alisema Kenya inawekeza katika miundombinu ya kisasa ya viwanja vya ndege, teknolojia ya kidijitali, usalama wa anga na mafunzo ya wataalamu ili kuimarisha nafasi yake kama kitovu kikuu cha usafiri wa anga kikanda na kimataifa.

Mudavadi alisema ukarabati na uboreshaji wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta, JKIA ni sehemu ya juhudi za kuboresha miundombinu ya usafiri wa anga nchini na kuongeza ushindani wa Kenya.

Aidha, Waziri huyo alisisitiza dhamira ya Kenya katika Soko Moja la Usafiri wa Anga Afrika, SAATM, akitoa wito wa kuimarishwa kwa sera za anga wazi.

Alisema muunganisho bora wa anga unaweza kupunguza gharama za usafiri huku ukichochea biashara, utalii, uwekezaji na ajira, sambamba na malengo ya Eneo Huru la Biashara Afrika, AfCFTA.

Mudavadi pia aliitaka sekta hiyo kutumia teknolojia mpya kama akili unde, usalama wa mtandao na mifumo ya kielektroniki, huku ikiandaa kizazi kijacho cha marubani, wahandisi na wataalamu wa usafiri wa anga.

Share This Article